Je, Tanzania inaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa urani duniani?

m

Chanzo cha picha, shutterstock.com

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Safari ya hivi karibuni ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan nchini Urusi, imefungua matumaini mapya ya Tanzania kuanza shughuli za uchimbaji wa madini ya urani kupitia uwekezaji wa makampuni kutoka Urusi.

Tanzania inajivunia utajiri wa madini ya aina mbalimbali na kuifanya kuwa nchi muhimu katika sekta hiyo duniani. Kuna madini ya vito vya thamani, madini ya viwandani, na madini mengine muhimu hasa katika maendeleo ya uzalishaji wa vifaa rafiki kwa mazingira.

Dhahabu ndio madini ya taifa kwa Tanzania, ikiiweka nchi hiyo miongoni mwa wazalishaji wakubwa barani Afrika. Zaidi ya dhahabu, Tanzania ina Tanzanite, madini yanayopatikana Tanzania pekee katika Milima ya Mererani karibu na Mlima Kilimanjaro.

Hivi karibuni Tanzania imegundua madini mengine muhimu ya Rare Earth Elements (REEs), aina ya Neodymium na Praseodymium, ambayo ni muhimu katika teknolojia ya kisasa; utengenezaji wa magari, chipu hadi vifaa vya hospitali.

Lakini leo tuna zungumzia madini mengine muhimu yaliyopo Tanzania, ambayo ni urani. Hadi Mei 205 Tanzania ina hifadhi ya takribani tani 58,500 za urani ambazo tayari zimethibitishwa, huku tafiti zaidi zikiendelea.

Urani ni nini?

Urani (au Uranium) ni kemikali au madini yenye metali nzito yenye mionzi, inayotumika kama chanzo cha nishati ya nyuklia duniani.

Matumizi maarufu ya urani hutumika kama mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia. Atomi zake zinapopasuliwa hutoa joto, ambalo hutumika kutoa mvuke, ambao huendesha mitambo, na kutoa umeme bila uzalishaji wa kaboni chafu.

Katika uwanda wa ulinzi, urani iliyorutubishwa kwa kiwango kikubwa hutumika kuzalisha silaha za nyuklia. Kuna nchi takribani tisa zenye silaha za nyukulia; Urusi, Marekani, China, Ufaransa, Uingereza, India, Pakistan, Israel na Korea ya Kaskazini.

Pia kuna matumizi ya kimatibabu na kisayansi. Vinu vya utafiti vinavyotumia urani hutoa mionzi inayotumika katika dawa kwa ajili ya kugundua na kutibu magonjwa kama saratani.

Mafuta ya urani hutumika katika mitambo ya majini ili kuendesha nyambizi na manowari za kubeba ndege. Na kwa sababu ya uzito wake, urani hutumika kuweka uwiano wa uzito katika vyombo vya angani na baharini.

Urani ya Tanzania

mk

Chanzo cha picha, Daily News

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Ndani ya nchi yetu Mungu ametubariki uraniamu (urani). Ni vyema kusimamia ule mradi wetu kule Namtumbo, wale wawekezaji waanze kazi sasa tufaidike na rasilimali ile."

Ni kauli ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa mwishoni mwa mwezi Mei, 2025.

Kulingana na Tasisi ya Nyuklia Duniani (WNA), mwaka 2024, uzalishaji wa urani duniani uliongezeka na Kazakhstan ilizalisha asilimia 39, ikifuatiwa na Canada asilimia 24 na Namibia asilimia 12. Uzbekistan ilichangia takriban asilimia 7, huku Urusi ikichangia kati ya asilimia 4 na 5 ya uzalishaji wa kimataifa.

Kwa mujibu wa serikali ya Tanzania, miradi ya urani haitahusishwa kwa njia yoyote na uzalishaji wa silaha za nyuklia bali itatumika kuzalisha nishati safi inayotumika katika mitambo ya nyuklia kote ulimwenguni.

Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Kutoeneza Silaha za Nyuklia (NPT), hivyo matumizi ya madini ya urani lazima yaendane na malengo ya amani na maendeleo endelevu.

Baada ya safari ya Urusi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji nchini Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo, amesema, "makampuni 13 ya Urusi yanafanya kazi nchini Tanzania kwa sasa, yakiwa na uwekezaji wenye thamani ya takriban dola milioni 400 za Marekani (zaidi ya trilioni 1), huku mradi unaoendelea wa urani wa Mkuju pekee ukitarajiwa kuchangia dola bilioni 1.2 za Marekani (zaidi ya trilioni 3.1) katika mtaji."

Kwa ujumla uchimbaji wa madini ya urani, unaiweka Tanzania katika nafasi ya kuvuna faida kubwa za kiuchumi na kimkakati. Kadri mahitaji ya kimataifa ya nishati safi yanavyoongezeka, kutaibadilisha nchi kuwa muhimu katika mazingira ya nishati ya kimataifa

Ndani ya nchi, mnyororo wa biashara hiyo utachochea maendeleo makubwa ya viwanda na uundaji wa ajira. Shughuli za uchimbaji zinatarajiwa kuunda maelfu ya ajira za moja kwa moja kwa wanajiolojia, wahandisi, na mafundi.

Fursa na Changamoto

Madini ya urani ni hatari sana kwa sababu yana mionzi ya nyuklia (Alpha, Beta, na Gamma) inayosababisha mabadiliko ya chembechembe hai (DNA) mwilini. Mionzi hii na sumu ya kemikali ya madini, huleta athari kadhaa.

Mionzi ikiingia hewani au kuingia mwilini kupitia vumbi na maji husababisha saratani (hasa ya mapafu na mifupa), na huharibu mfumo wa uzazi, hivyo kusababisha watoto kuzaliwa na ulemavu.

Uchimbaji wake huacha vifusi vyenye mionzi ambavyo huweza kusambaa kupitia upepo, mvua, na mito, na hivyo kuchafua maeneo ya makazi na malisho kwa miaka mingi.

Urani iliyorutubishwa hutumika kutengeneza silaha za maangamizi kama mabomu ya nyuklia, ambayo yana uwezo wa kuua maelfu ya watu na kuacha mionzi itakayodhulumu vizazi vijavyo.

Urani ni fursa kubwa kwa Tanzania katika kukuza uchumi wake, lakini fursa hii ni lazima iende sanjari na kuzingatia athari zake kwa binadamu na mazingira. Kwa lugha nyingine, urani haipaswi kuwa utajiri unaouwa Watanzania.