Watoto wa umri wa miaka 9 wanaangalia ngono - Utafiti
Na Shiona McCallum, Ripota wa Teknolojia

Chanzo cha picha, Getty Images
Watoto wanaangalia video chafu za ngono mtandaoni kuanzia umri wa miaka tisa, kwa mujibu wa utafiti wa kamishna wa watoto nchini Uingereza.
Utafiti huo unaonyesha pia robo ya vijana wenye umri wa miaka 16-21 waliangalia picha hizi kwa mara ya kwanza kwenye mtandao wakiwa bado wako shule ya msingi. Kufikia umri wa miaka 13, asilimia 50% walikuwa tayari wameangalia.
Matokeo hayo yamehusishwa na kutojistahi miongoni mwa vijana na mitazamo hatarishi kuhusu ngono na mahusiano.
Kamishna Dame Rachel de Souza alisema "ni tatizo".
Katika utafiti huo wa kitaifa uliohusisha watu 1,000 wenye umri wa kuanzia miaka 16-21, asilimia 38% walikutana na maudhui ya video za ngono kwa bahati mbaya.
Mtoto wa Joanne Schneider alikumbana na tovuti ya ngono, akiwa na umri wa miaka minane, baada ya kuandika mtandaoni maneno ya matusi aliyoyasikia shuleni.
"Tuliweka vitu vyote vya kawaida vya usalama na tukaondoa programu kama vile YouTube lakini hatukufikiria hata sekunde moja kuwa mwanangu anaweza kujikuta kwenye tovuti za burudani za watu wazima ndani ya sekunde chache," Bi Schneider, kutoka London, sema.
"Mara tu nilipoona kile kilichokuwa kikitendeka, nilifunga tovuti - lakini yeye na mimi tulibaki katika mshtuko kwa kile alichokiona. Nilijisikia vibaya sana juu ya jambo hilo zima.
"Ghafla nililazimika kuelezea yote, pamoja na ukweli kwamba kile alichokiona kilikuwa ni maigizo na ni tofauti na jinsi watu halisi wanavyoonekana."
Kuonekana ni kama jambo la kawaida
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kati ya vijana wenye umri wa miaka 18-21, asilimia 79% walikuwa wameangalia video chafu zinazohusisha unyanyasaji wa kijinsia wakiwa watoto.
Takribani nusu ya vijana wanasema wasichana wanatarajia kitendo cha kujamiiana kuhusisha unyanyasaji wa kimwili, ripoti ya kamishna inasema.
Mtoto mmoja wa miaka 12 alimwambia Dame Rachel kwamba mpenzi wake "alimnyonga" wakati akimbusu kwa mara ya kwanza. Alikuwa ameiona hivyo kwenye mtandao wa ngono "na akafikiri ni kawaida".
Kamishna anahimiza "kila mtu mzima ana nafasi ya kuwajibika" na kuchukulia kwa uzito matokeo hayo.
Mswada wa Usalama Mtandaoni, unaopitia bungeni, unapaswa kutumiwa kuwalinda watoto dhidi ya video za ngono mtandaoni, anasema.
"Isiwe hivyo kwamba watoto wadogo wanakumbana na video za ngono zenye ukatili na chuki dhidi ya wanawake kwenye tovuti za mitandao ya kijamii," Dame Rachel anasema.
"Ninaamini kweli tutaangalia nyuma katika miaka 20 na kushtushwa na maudhui ambayo watoto walikuwa wakionyeshwa.
"Maudhui ya watu wazima ambayo wazazi wanaweza kufikia katika ujana wao yanaweza kuchukuliwa kuwa 'ya ajabu' kwa kulinganisha na ulimwengu wa kisasa wa video za ngono mtandaoni."
Dame Rachel aliwahimiza wazazi kutokwepa mazungumzo kuhusu suala hili nyumbani na kuweka wazi kuhusu video za ngono zilivyokithiri maudhui "yasiyo ya kweli, ni ya kuigiza".
Aliwaambia watoto kupitia BBC Breakfast "wanataka mama na baba wazungumze na watoto wao mara kwa mara, hata wakiwa wachanga sana, kwa njia inayolingana na umri kuhusu mambo ambayo wanaweza kuona ili wasichanganyikiwe".
Alisema mazungumzo kuhusu "mipaka rahisi" kama vile kwa nini inaweza kuwa si sawa kwa vijana kuwa na simu zilizounganishwa kwenye mtandao au akaunti za mitandao ya kijamii pia ni jambo muhimu.
Kudhibiti maudhui makali
Shirika la Kitaifa la Kuzuia Ukatili kwa Watoto kwa muda mrefu limekuwa likihimiza serikali kutekeleza hatua kali katika Mswada wa Usalama Mtandaoni ili kuwalinda watoto.
Kiongozi wa sera Richard Collard alisema athari ambayo video za ngono inaweza kuleta "inatia wasiwasi sana".
"Ofcom lazima ipewe mamlaka ya kuweka viwango vya chini ambavyo vinahakikisha kuanzishwa kwa hatua kali za uhakikisho wa umri kwenye mitandao ambayo video za ngono zinaweza kutazamwa," alisema.
"Hii itahakikisha watoto wanalindwa dhidi ya madhara ya mara moja na ya baadaye."
Andy Lulham, kutoka kwa mtoa huduma wa teknolojia ya usalama VerifyMy, alisema ripoti hiyo "inatia wasiwasi sana lakini cha kusikitisha haishangazi".
"Kwa hali ilivyo, hakuna kitu cha kuwazuia watoto kupata video za ngono na maudhui mengine makali mtandaoni," alisema.
"Suala hili limekuwepo kwa muda mrefu sana - ni wakati wa wanasiasa, wasimamizi na sekta binafsi hatimaye kuja pamoja na kusaidia kulinda watoto, sehemu iliyo hatarini zaidi ya jamii."












